Jumatano, 18 Desemba 2013

UMESHAGUNDUA ANACHOHITAJI MWENZI WAKO?-


KUJUA anachohitaji mwenzako ni kila kitu katika uhusiano na ni vyema basi kila wakati kujifunza mbinu za kuendelea kuwa bora zaidi kwa mwenzi wako. Yes! Hapa katika All About Love ni sehemu sahihi ya kukuza uelewa wako.

Tunapitia mambo muhimu ambayo wanawake wengi huvutiwa nayo kwa wanaume. Kuyajua kutakufanya uendelee kuwa mbabe kwenye sayari hii. Ni mada yenye lengo la kuwasaidia zaidi wanaume ambao hawafahamu ni nini hasa wanawake wanapenda kutoka kwao.

Kwa bahati mbaya, wanaume wengi hawapati muda wa kutosha kufikiria kuhusu mapenzi – wengi wanaishia kujadili kuhusu ngono! Hili ni tatizo. Ngono haiwezi kuwa yenye furaha kama uhusiano unayumba.

Ngoja niwaambie, tendo la kukutana kimwili, siyo kila kitu kwenye uhusiano. Upendo ndiyo kila kitu katika mapenzi rafiki zangu. Si vibaya kuwaza namna ya kumfurahisha mwenzako, lakini iwe ndani ya mambo mengine mengi katika kujenga na kuimarisha penzi lenu.
Hebu sasa tuendelee na mada yetu...

MSIFIE MWENZAKO
Wanaume wengi hupuuzia hili, huona kama ni jambo lisilo na maana sana kwao na wenzi wao. Hali ni tofauti sana kwa wanawake ambao hupenda kuwasifia wanaume zao. Nitakupa mifano miwili ya namna wanandoa wa jinsia mbili tofauti wanavyotambulishana kwa jamaa zao.

MWANAUME: “Peter kutana na mke wangu, anaitwa mama Diana. Nipo naye mwaka wa tatu sasa, tuna watoto wawili, huyo Diana na mwingine anaitwa Chris. Mama Diana, huyu ni Peter nilisoma naye Tosamaganga Sekondari.”
MWANAMKE:“Suzan, huyu ndiye mume wangu mpenzi...anaitwa Elifaraja lakini mimi napenda zaidi kumuita Elly. Nampenda sana mume wangu jamani, tuna watoto wawili, Diana na Chris... (Akimgeukia mumewe) Baby, huyu hapa ni rafiki yangu Suzan. Yaani tumekua naye mtaa mmoja huko Arusha.”

Bila shaka kwa namna wawili hao walivyotambulishana unaweza kuona tofauti kubwa. Mwanaume amemtambulisha mkewe kawaida kabisa, hajaonesha manjonjo au namna anavyompenda na kumthamini, lakini mwanamke amefanya hivyo.
Sikia nikuambie, kumsifia mwanamke, kuna nafasi kubwa sana kwake. Chunguza kwa makini, hata kunapokuwa na mgongano katika familia, halafu wanakatokea wageni, baada ya utambulisho na mazungumzo ya hapa na pale, wageni wakiondoka kunakuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kumaliza mpasuko katika familia.

Jenga utamaduni wa kumsifia mpenzi wako, unamuweka katika kilele cha upendo. Anajiona kamili, peke yake na mwenye nguvu kwako. Anajiamini na unamfanya azidi kukupenda kwa kuwa anaamini yupo na mwanaume ambaye anajivunia kuwa naye.

MALENGO
Wanaume wengi wana ulemavu mmoja; hawapendi kuwashirikisha wanawake katika mambo yao. Wanapenda kufanya mambo yao kwa siri na wakati mwingine ikilazimika kumwambia mkewe basi kwa mshtukizo baada ya kukamilisha jambo husika.
Hii si sahihi. Dunia ya leo imebadilika rafiki zangu. Inawezekana wazee wa zamani walikuwa sahihi, maana ilikuwa ni suala la kununua ng’ombe na kuwaweka katika zizi kwenye kijiji cha jirani, halafu wanapewa malisho mazuri, baada ya miaka miwili wanazaliana, hapo ndipo anamweleza mkewe.

Siku hizi dunia imebadilika, kuna mambo mengi. Kuna suala la hasara katika biashara, utapeli n.k. Mkeo ndiye rafiki yako mkubwa kuliko wote, ndiye ndugu yako wa karibu zaidi kuliko yeyote. Mmeshirikiana kuzaa watoto na kujenga maisha pamoja.
Yeye anapaswa kujua mambo yako, ndiye mtetezi wako nambari wani. Mweleze juu ya malengo yako, wakati mwingine anaweza kukusaidia sehemu ambayo hukutarajia.

Hata hivyo, kumshirikisha katika malengo yako, kunampa nguvu na nafasi ya kujiona mama katika familia yenu. Msaidizi kamili wa nyumba.

KIPAUMBELE
Kuna wakati wanawake huwa na mambo yao binafsi. Kazini au kifamilia. Inawezekana akatatizika katika eneo fulani ambalo kwa namna moja ama nyingine atahitaji usaidizi wako. Ikitokea mkeo akawa katika hali hiyo, msikilize.
Mathalani ana tatizo la kifamilia, amekuambia mmoja wa wazazi wake anaumwa, msaidie. Si lazima kifedha, lakini kuonesha kujali kwako tu, kutampa matumaini kwamba anaishi na mtu sahihi. Acha kupuuza mambo yake; hata yale madogo, kama ya ‘mtoto wa dada amerudishwa ada shuleni’.

Msikilize, mshauri panapofaa kufanya hivyo na ukiweza msaidie hata kifedha. Katika upande wa pili ni hivyo hivyo. Labda una tatizo binafsi, kikazi au kifamilia, mshirikishe.
Unaweza kushangaa jambo ambalo uliamini unaweza kulimaliza peke yako, kwa kumshirikisha likawa jepesi zaidi na mambo yakaenda vyema. Kipaumbele kwa namna yoyote ile, kunaongeza mapenzi zaidi kwa mwanamke.

TENDO LA NDOA
Hiki ni kipengele nyeti, kinachohitaji lugha nzuri ya kirafiki kukifafanua. Hakuna siri, tendo la ndoa ni moja ya kiwakilishi cha ndoa. Maana hata maandiko yanasema: “Mwanamke ataacha wazazi wake na kwenda kwa mumewe, nao watakuwa mwili mmoja.”

Kimsingi tendo la ndoa lina nafasi yake. Ni muhimu likaheshimiwa na kutengewa muda maalum wa kufurahia. Si papara. Kwa bahati mbaya wanaume huwa si wafuatiliaji sana wa kujua namna ya kuwafurahisha zaidi wenzao. Wenyewe wanajiwazia wenyewe. Wanafikiria namna ya kuwakomoa wenzao.

Si sahihi. Tendo la ndoa halina maana ya kukomoana. Jenga mazoea ya kufanya maandalizi kamili kabla ya tendo. Sikiliza hisia za mwenzako. Ukiweza kumjulia mke wako katika eneo hili, ni wazi kwamba utazidisha upendo wake kwako, lakini pia atakuwa katika kuta za uaminifu. Akatafute nini nje wakati wewe ndiye mganga wake unayeweza kumtibu barabara?

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni