VMM/U.80/8/Vol.I/55 20/09/2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati ya Utekelezaji ya
Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa imekutana
Jumatatu Tarehe 19/09/2016 katika Ukumbi wa UVCCM Makao Makuu, Dar es Salaam
chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Sadifa Juma Khamis (MCC)(MB). Kikao hicho
kilitanguliwa na kikao cha Kamati ya Maadili na Nidhamu ya UVCCM Taifa, pamoja
na mambo mengine kilipokea na kujadili Uhai wa Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya
ya Vijana Mkoani Arusha.
Kikao kilipokea Taarifa na
kutafakari, kujadili na kufanya maamuzi yafuatayo:-
1. NDUGU LENGAI OLE SABAYA MWENYEKITI WA
UVCCM MKOA WA ARUSHA
Kwa
nyakati tofauti Ndugu Sabaya alisimamia na kuyaongoza makundi ya Vijana wa CCM
na wasiokuwa wa CCM ili kumkataa Katibu wa UVCCM aliyehamishiwa Mkoani Arusha Ndugu Said Goha kuchukua nafasi ya Ndugu Ezekiel Mollel licha ya yeye kupewa
heshima na kuelimishwa na Vikao vya Taifa na Viongozi mara kadhaa kupitia
Mwenyekiti wa UVCCM Taifa kuhusu mamlaka za Kikanuni, Kanuni ya UVCCM Kanuni ya
Utumishi na Kanuni ya Maadili.
Ndugu
Sabaya amesababisha taharuki iliyopelekea Ofisi ya UVCCM Mkoa wa Arusha
kufungwa kwa minyororo hadi Jeshi la Polisi kuingilia kati. Vile vile taharuki
hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa Vijana wa Mkoa wa Arusha kugawanyika katika
makundi na kupelekea hali ya Kiusalama na Maadili kwa Jumuiya na Chama kuwa ya
wasiwasi.
Ndugu
Sabaya kufikishwa Mahakamani akikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la
kujifanya Mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa. Huku kosa la pili katika muda
usiojulikana akidaiwa kughushi vitambulisho vya Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) chenye namba MT 86117 wakati
akijua ni kinyume cha Sheria za nchi.
Kamati
ya Utekelezaji ilipitia tuhuma mbali mbali za vielelezo vya utapeli na ulaghai unaodaiwa
kutendwa na Ndugu Lengai Sabaya katika maeneo tofauti huku akijua ni kinyume na
miiko ya Maadili ya Uongozi wa UVCCM na CCM.
Kwa
makosa yote hayo Ndugu Lengai Ole Sabaya ameyafanya kwa kukiuka Kanuni ya
Uongozi na Maadili ya CCM Fungu la (3) ukurasa wa 16 na 17, na fungu la nne (4)
ukurasa wa 29, 30 na 31. Pia makosa hayo ameyatenda kinyume na taratibu za
Uongozi na Maadili za UVCCM, Ibara ya 6.3.2 Ibara ya 7.5.1, 7.5.4 na 8.2.5.
Kamati
ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Taifa imependekeza kwa
Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) kumvua uongozi Ndugu Lengai Ole Sabaya,
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha.
Wakati
tukisubiria maamuzi ya Chama Cha Mapinduzi, Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu
la UVCCM Taifa imemsimamisha Uongozi wa Nafasi yake ndani ya UVCCM kutokana na
kesi iliyoko Mahakamani na kumtaka kuanzia leo tarehe 20/09/2016 asijihusishe
na shughuli zozote za Uongozi wa UVCCM hadi hatima ya tuhuma zake
itakapoamuliwa na Mahakama na Vikao husika vya UVCCM na CCM.
2. NDUGU EZEKIEL MOLLEL
Ndugu
Ezekiel Mollel alipokuwa Katibu wa Vijana Mkoa wa Arusha alipewa barua ya
Uhamisho, kama inavyoelekezwa na Kanuni ya Utumishi ya UVCCM kifungu cha 3(13)
ukurasa wa 21 na 22 inayozungumzia Uhamisho wa mtumishi, Nukuu
“Mfanyakazi
yeyote atakayekataa kutii amri ya Uhamisho bila sababu zinazokubalika
atachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni hizi”, kama ilivyo katika
kifungu cha 7(4)(b)(x). Katika kifungu hiki yameainishwa makosa mengi lakini
aliyoyatenda Ndugu Mollel ni haya yafuatayo:-
Kuachishwa na Kufukuzwa Kazi”
Nukuu “Mfanyakazi yeyote wa UVCCM ikithibitika kuwa amefanya mojawapo ya makosa
yafuatayo ataachishwa Kazi”
(i)
Kuwa ni mwenye hatia ya kitendo cha ukosefu
wa Adabu mahali pa kazi au wakati wa kazi.
(ii)
Kwa makusudi kukataa kutii amri/maagizo
halali ya Wakuu wa Kazi au kukataa kutii amri ya Uhamisho.
(iii)
Kushiriki kwa njia moja au nyingine katika
kutenda mambo yaliyo kinyume na Maadili ya Uongozi UVCCM na CCM.
Makosa
haya ameyarudia Ndugu Ezekiel Mollel aliwahi kusimamishwa kazi mwaka 2015 akiwa
Katibu wa UVCCM Mkoa wa Manyara, jambo ambalo lilipelekea kumnyang’anya Kituo
na Kumsimamisha Kazi kwa muda, pamoja na yote hayo bado Ndugu Ezekiel Mollel hakuweza kujirekebisha hata pale aliporudishwa
Kazini na kupelekwa Mkoa wa Arusha.
Kamati
ya Utekelezaji ya UVCCM Taifa imebariki maamuzi yaliyochukuliwa na Sekretarieti
ya Baraza Kuu ya UVCCM Taifa iliyokutana tarehe 14/09/2016. Kamati ya
Utekelezaji ya UVCCM Taifa imependekeza kwa Baraza Kuu la UVCCM Taifa kumfukuza
Kazi mara moja Ndugu Ezekiel Mollel.
TUHUMA ZA KUIBUA UFISADI
Kuhusu
madai ya tuhuma zinazotolewa na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha kuwa kuna
ufisadi na baadhi ya Viongozi wa Makao Makuu ya UVCCM Taifa wanahusika.
Ikumbukwe
kuwa Umoja wa Vijana wa CCM ulianza kujitathimini na kuhakiki Mali za Jumuiya
tokea mwezi Desemba, 2015.
Umoja
wa Vijana wa CCM Taifa kwa agizo la Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. John Pombe
Magufuli alilolitoa mwezi Julai, 2016 ulikamilisha uhakiki wa Mali zote za
UVCCM Taifa, Mikoa na Wilaya na kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi.
Mkoa
wa Arusha ni miongoni mwa Mikoa
iliyobainika kuwa taarifa zake hazikuwa na ukweli na kubainisha matakwa
ya uhakiki kama walivyoagizwa.
Kikao
cha Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa kilichokutana tarehe
18/08/2016 Mjini Dodoma kupokea na kupitia taarifa za uhakiki Mali za UVCCM
ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya kiliagiza Sekretarieti ya Baraza Kuu la UVCCM
Taifa kuwaita Viongozi wa Mkoa wa Arusha ili kuendelea kujiridhisha na taarifa
walizowasilisha Makao Makuu kwa vile zimebainika kuwa na mapungufu makubwa.
Katika
Taarifa hiyo iliyowasilishwa kwa maandishi na kuthibitishwa na Kamati ya
Utekelezaji ya Mkoa wa Arusha hakuna sehemu ambayo kumeainishwa ubadhirifu ama
upotevu wa fedha kinyume na madai yaliyoibuliwa siku za karibuni baada ya
Viongozi hao kuchukuliwa hatua za kinidhamu, kutokana na makosa ya Maadili ya
Uongozi.
Hata
Kamati ya Utekelezaji ya Mkoa wa Arusha ilipoitwa katika kikao cha Kamati ya
Maadili cha tarehe 19/08/2016 kilichofanyika Mjini Dodoma walikana na kudai wao
hawajawasilisha malalamiko yoyote kuhusu tuhuma wanazozitoa na kusema
wanaendelea na kufanyia kazi na kurekebisha mambo ya msingi kuhusu Uchumi wa
Mkoa wao.
Kufuatia
hatua hiyo Kamati ya Maadili na Nidhamu na Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu
la UVCCM Taifa iliagiza Ofisi ya Katibu Mkuu iendelee kufuatilia kwa karibu
jambo hilo ili kubaini ukweli baada ya kujiridhisha kuweko na harufu ya
ubadhirifu, jambo ambalo limepelekea Viongozi hao kutosema ukweli pamoja na kusisitizwa
mara kadhaa kwa maandishi bado taarifa zao hazikujitosheleza.
Ofisi
ya Katibu Mkuu ilitoa miongozo ya uhakiki kupitia barua Kumb. Na. VMM/C/C.30/15/77 ya tarehe 6/04/2016 na VMM/C/C.30/15/107 ya tarehe 28/07/2016
na VMM/C/C.30/15/112 ya tarehe 29/07/2016.
Kamati
ya Utekelezaji imeagiza Sekretarieti kuendelea na hatua zake za kufuatilia
jambo hilo na taarifa iwasilishwe haraka iwezekanavyo.
Kamati
ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa imeteua wajumbe watatu wakiongozwa
na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Mhe. Mboni Mhita (MB)(MNEC) kufuatilia kwa
karibu suala la Arusha na taarifa iwasilishwe katika vikao husika.
Kamati
ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa imeendelea kusisitiza UVCCM ni
Taasisi kubwa hivyo uendeshaji wake wa kazi ni uzingatiaji wa Kanuni, Taratibu
na Miongozo hivyo haitamkingia kifua mtu katika jambo ambalo linahatarisha uhai
au uhujumu wa rasilimali za Jumuiya.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka
Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni